Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Ustahimilivu wa Yemen, kama ngome kuu ya msaada wa kijeshi kwa watu wa Gaza, umeendelea kusimama imara licha ya taifa hilo kuendelea kuwa chini ya mzingiro na hali ngumu ya kiuchumi.
Wananchi wa Yemen kutoka nyanja mbalimbali – wakiwemo wanahabari, wahadhiri, wanafunzi wa shule na vyuo vikuu – wamesimama bega kwa bega na watu wa Gaza katika kuwatetea.
Baada ya kupokea mashambulizi makali kutoka kwa nguvu za anga, makombora, na ndege zisizo na rubani za Yemen – pamoja na kufungwa kwa bandari muhimu kama Eilat, na kudhoofika kwa uchumi wake kutokana na marufuku ya meli za Kizayuni katika mlango bahari wa Bab al-Mandeb – utawala wa Kizayuni umejibu kwa mashambulizi ya angani dhidi ya raia na maeneo yasiyo ya kijeshi, bila kujali sheria yoyote ya kimataifa, na kuua makumi ya raia wa Kiyemeni.
Katika mashambulizi haya, waandishi wa habari wa Yemen – licha ya kuwa na kinga ya kimataifa – walilengwa moja kwa moja na utawala wa Kizayuni na kuuawa shahidi.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Al-Masirah kutoka Yemen, zaidi ya waandishi wa habari 32 waliuawa shahidi wiki iliyopita (Jumatano), katika mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni – mashambulizi ambayo yalikuwa miongoni mwa ya kinyama na ya kutisha zaidi. Israel ilishambulia mitaa ya raia, maeneo ya kihistoria, na watu wasiokuwa na hatia bila kutoa sababu yoyote. Dunia nzima iliona jinsi adui huyo alivyoidharau mipaka yote na hakuheshimu hata "mistari myekundu" ya sheria za kimataifa.
Mashujaa waliouawa kutoka magazeti kama "26 Septemba" na "Al-Yemen" walikuwa "kikundi chenye kung'aa kwa taji la ushahidi – wanaume wa kalamu, wanaume wa ngome ya neno lenye nuru." Walipaa wakisimama katika "uwanja wa maneno", wakiupinga adui na mradi wa kiharibifu wa uvamizi wa kimataifa unaoongozwa na Marekani, hadi wakapata shahada yao.
Yemen leo imeaga kundi la waandishi wa habari waliouawa shahidi katika shambulio la kikatili - shambulio kubwa zaidi dhidi ya uandishi wa habari na waandishi katika historia ya Yemen.
Baada ya kuswaliwa kwa miili ya mashahidi katika Msikiti wa Al-Shaab uliopo katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Sana’a, mji mkuu wa Yemen, ibada ya mazishi ilifanyika kwa mahudhurio makubwa ya wananchi, kisha mashahidi walihamishiwa kwenye makaburi yao ya milele.
Wale waliowashindikiza mashahidi katika mazishi walisisitiza kuwa iwapo mauaji haya ya kinyama ya waandishi wa habari yangefanyika katika nchi nyingine yoyote, basi dunia ingeripuka kwa haraka na kwa sauti kubwa. Walikosoa vikali vigezo viwili vya maadili vinavyotumiwa na jumuiya ya kimataifa – ambavyo huendesha maamuzi kwa mujibu wa maslahi ya mataifa ya kihalifu duniani, wakiongozwa na "Shetani Mkuu" (Marekani) na mkono wake wa Kizayuni (Israel).
Walisema kuwa kimya cha jumuiya ya kimataifa kinadhihirisha ushirikiano wa kimya kimya katika shambulio hili la damu na jinai.
Mazishi haya – ya kitaifa na ya wananchi – yameonyesha kwa dhahiri nafasi muhimu ya waandishi wa habari katika kukabiliana na uvamizi, na kueleza ufahamu wa kina wa hatari ya "vita ya vyombo vya habari", ambayo si ndogo wala dhaifu ukilinganisha na mapambano ya kijeshi uwanjani.
Kwa upande mwingine, mwandishi wa Al-Masirah kutoka Gaza ameripoti leo huku mashambulizi ya mabomu yakizidi ukali. Du’a Ruqa, mwandishi wa televisheni ya Al-Masirah huko Gaza, katika ripoti yake alisimulia simulizi ya familia yake, ambapo licha ya yeye mwenyewe kuhamia kusini ili kufuatilia matukio, familia yake ilibaki mjini Gaza.
Alisisitiza kuhusu mshikamano wa kishujaa wa wakazi wa Ukanda wa Gaza, na akaeleza kuwa mama yake, pamoja na maelfu ya wengine, wamekataa kuondoka mjini humo, wakipaza kauli mbiu: "Kifo badala ya kuhamishwa kwa nguvu."
Ruqa, katika mahojiano yake na televisheni ya Al-Masirah kwenye kipindi cha “Madirisha”, alieleza kuwa mashine ya vita ya Kizayuni inaendelea na mashambulizi ya kikatili dhidi ya Ukanda wa Gaza, yakiambatana na uharibifu mkubwa, ongezeko la idadi ya mashahidi na watu waliopotea chini ya vifusi.
Alisema kuwa hali ya kwenye uwanja ni ngumu sana, na akasisitiza kuwa kwa sababu bado kuna watu waliokwama chini ya mabaki ya nyumba zilizobomolewa, idadi halisi ya mashahidi bado haijajulikana.
Aidha, alibainisha kuwa utawala wa Kizayuni umeongeza mashambulizi yake ya kijeshi ndani ya jiji la Gaza, jambo ambalo limesababisha ongezeko la kila siku la vifo. Katika saa za awali za leo, watu 41 wameuawa, ambapo 37 kati yao walikuwa ndani ya jiji la Gaza. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka huku vikosi vya uokoaji vikiendelea kuwatafuta waliokwama chini ya vifusi.
Mwandishi wetu kutoka Gaza aliongeza kuwa mashambulizi ya anga na makombora yanaendelea bila kukoma, huku ndege za kivita na za upelelezi zikizunguka katika maeneo yenye watu wengi, hasa katika maeneo ya kaskazini, magharibi na kusini-magharibi, kama vile Tel Al-Hawa. Maeneo haya, ambayo yamejaa wakazi na wakimbizi wa ndani, sasa yametangazwa kuwa "maeneo mekundu", kwa lengo la kuwalazimisha wakazi kuhama kuelekea upande wa kusini wa Ukanda wa Gaza.
Mwandishi huyo pia alisisitiza kuwa, licha ya mabomu yanayoendelea, wengi wa wakaazi wa Gaza wamekataa kuondoka katika jiji hilo, wakisema wanapendelea kufa kuliko kupitia tena mateso ya kuhama kwa nguvu kama ilivyotokea Oktoba 2023. Ingawa sehemu kubwa ya wakazi wamekimbia kutokana na mashambulizi, bado kuna familia nyingi zilizoamua kubaki na kushikamana na ardhi yao.
“Watu wa Gaza hawategemei kitu chochote - si mikutano ya Waarabu, wala msaada mwingine wowote.” Mwandishi wa Al-Masirah alieleza kuwa Wapalestina wa Gaza wameonyesha aina ya kipekee ya uthabiti na msimamo, bila kutegemea msaada wa nje. Baada ya kushuhudia mikutano ya Waarabu ambayo haikutoa chochote zaidi ya matamko matupu, watu wa Gaza hawana matumaini kwa yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu na mshikamano wao na ardhi yao.
Katika hitimisho la ripoti yake, mwandishi alisema kuwa watu wa Ukanda wa Gaza ni mfano wa kipekee wa uvumilivu na msimamo mbele ya “mashine katili zaidi ya mauaji katika historia”. Wanakabiliana na hali zote za mateso – kutoka kwa mashambulizi ya mabomu, uharibifu mkubwa wa miundombinu, hadi njaa – kwa roho ya kupambana isiyopungua.
Pamoja na mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Yemen yanayoendelea, waandishi wa habari wa Yemen, kama raia wengine na serikali ya Sana’a, wameapa kuendelea kuunga mkono na kuwatetea watu wa Gaza hadi mashambulizi ya Israel dhidi ya watu hao madhulumu na jasiri yatakapokoma.
Your Comment